Ikisiri: Utafiti huu, ulichunguza dhima za maana za kipragmatiki katika tambo za mashabiki wa mpira wa miguu, kwa kuzingatia mifano kutoka kwa mashabiki wa timu za Simba na Yanga. Maana za kipragmatiki zina nafasi muhimu katika kufafanua ujumbe uliokusudiwa na wazungumzaji kulingana na muktadha wa matumizi ya lugha. Katika tambo za mashabiki wa mpira, maana hizi hutumika kuonesha hisia, mitazamo, utambulisho wa mashabiki, ushindani na msimamo wao dhidi ya timu pinzani. Aidha, tambo hizo zinaweza kutumika katika kuhamasisha timu, kujenga mshikamano miongoni mwa mashabiki, kudhihaki wapinzani na kuonesha kujiamini kuhusu ushindi wa timu zao. Utafiti huu ulitumia mkabala wa kitaamuli katika ukusanyaji na uchanganuzi wa data. Data zilichanganuliwa kwa kuzingatia muktadha wa matumizi ya tambo na maana zinazokusudiwa na mashabiki. Pia, katika kujibu maswali ya utafiti, ilitumika Nadharia ya urekebishaji mawasiliano kama mwongozo wa kutafuta ufumbuzi wa tatizo. Matokeo ya uchambuzi yanaonesha kuwa tambo hizo hubeba na kuwasilisha dhima mbalimbali za kipragmatiki zinazochangia katika ujenzi na uimarishaji wa mawasiliano ndani ya makundi ya mashabiki. Dhima ya kwanza ilikuwa ni dhima ya utambulisho na mshikamano wa kikundi, dhima ya kuhamasisha na kuchochea hisia, dhima ya burudani na ucheshi wa lugha na mwisho dhima ya ubunifu wa lugha. Matokeo pia yalionesha kuwa maarifa ya awali ya wasikilizaji kuhusu timu, wachezaji, historia ya mechi na ushindani uliopo kati ya timu mbalimbali husaidia kufasiri ujumbe uliokusudiwa katika tambo. Hivyo, tasnifu hii ina mchango mkubwa katika taaluma ya Isimu ya Kiswahili na inatarajiwa kuongeza uelewa kuhusu nafasi ya pragmatiki katika kuchambua lugha inayotumiwa na mashabiki wa mpira wa miguu na namna lugha hiyo inavyotekeleza dhima mbalimbali za kimawasiliano katika jamii.
Title: Dhima za Maana za Kipragmatiki katika Tambo za Mashabiki wa Mpira
Author: Emiliana Orest Ngowi, Dkt. Mussa Omary Amanzi
International Journal of Social Science and Humanities Research
ISSN 2348-3156 (Print), ISSN 2348-3164 (online)
Vol. 14, Issue 4, October 2026 - December 2026
Page No: 122-133
Research Publish Journals
Website: www.researchpublish.com
Published Date: 16-October-2026